Idara ya usalama imelaumiwa kwa kutochukua hatua za kisheria kwa washukiwa wa mauaji ya watu takribani 12 katika visiwa tofauti Kaunti ya Lamu na kaunti nyenginezo mkoani Pwani.
Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa baraza la maimamu hapa nchini Sheikh Abdalla Ateka, alipokuwa akihutubia waandishi wa habari siku ya Jumanne katika eneo la Kikambala baada ya kufanya kongamano na wakuu wa baraza hilo kutoka kaunti tofauti humu nchini wakijadili suala la usalama.
Ateka aliongeza kuwa mauwaji hayo yanasababishwa na kuongezeka kwa vijana wengi wanaotumia dawa za kulevya, na kusisitiza kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi kuna uwezekano wa kushuhudiwa mauwaji zaidi.
Aidha, aliitaka idara ya usalama mkoa wa pwani kushirikiana katika kukabiliana na janga la mihadharati na mauwaji ya kiholelaholela, na kuongeza kuwa watakaopatikana, sharti wakabiliwe kisheria.
Wakati uo huo, katibu mtendaji wa baraza hilo Mohamed Abdulkadir aliitaka serikali kuongeza vituo vya polisi katika kaunti ya Lamu na mkoa mzima wa Pwani ili usalama uweze kuimarika kwa wananchi.