Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewaonya wahudumu wa teksi dhidi ya kuwasafirisha wahalifu.
Akihutubu kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumatatu alipofanya kikao na washikadau wa idara ya usafiri, Onunga alisema kuwa afisi yake inaendelea kuchunguza madai kuwa madereva wengi wa teksi wamekuwa wakiwasafirisha wahalifu hasa masaa ya usiku.
Onunga alisema imekuwa vigumu kwa maafisa wa polisi kuwanasa wahalifu kwa kuwa baada ya wahalifu hao kutekeleza wizi, magari hayo ya teksi huwaondoa kwa haraka katika maeneo hayo.
"Afisi yangu imeanzisha uchunguzi kubaini madereva wa teksi wanaotumika kuwasafirisha wahalifu hasa majira ya usiku baada ya kuwapora wenyeji wa kaunti hii. Wanaojihusisha katika uhalifu huo wajue kuwa siku zao zimehesabiwa,” alisema Onunga.
Kamishna Onunga aliwahimiza madereva wa teksi kushirikiana na maafisa wa polisi ili kukabilina na visa vya uhalifu akisisitiza kuwa sharti wananchi wajitolee kushirikiana na vyombo vya usalama ikiwa uhalifu utakabiliwa Nyamira.
"Nawaomba madereva wa teksi kushirikiana na maafisa wa polisi ili kusaidia kukabili visa vya uhalifu vinavyo ripotiwa mara kwa mara kwa kuwa pasina ushirikiano wa aina hiyo, basi itakuwa vigumu kukabiliana na janga hili," alisema Onunga.