Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi katika eneo la Katine, kaunti ndogo ya Matungulu, wameonywa dhidi ya kuwahusisha watoto wao katika uuzaji wa pombe haramu shule zitakapofungwa.

Akizungumzia katika ofisi yake siku ya Ijumaa, chifu wa Tala Pius Nzioka alielezea kuwa visa vya watoto wadogo kuuza pombe haramu huongezeka wakati wa likizo.

Chifu huyo alielezea kuwa wazazi watakaopatikana wakikiuka onyo hilo watafunguliwa mashtaka ya kuuza pombe haramu pamoja na kukiuka haki za watoto.

"Wazazi wengi wanaouza pombe haramu hupenda kuwahusisha wanao katika biashara hiyo bila kujua kuwa watoto hawa wana haki zao zinazopaswa kutiliwa maanani,” alisema Nzioka.

Nzioka alisema kuwa wazazi wanapowahusisha wanao katika biashara ya uuzaji wa pombe haramu, huwa wanawatia wanao katika hatari ya kuanza kutumia pombe hiyo na hivyo kuathiri masomo pamoja na fikira zao.

Aliwaomba wazazi kuwa kielelezo chema kwa watoto wao ili wawe watu wa kufana katika jamii.