Wakaazi wa eneo bunge la Bahati katika kaunti ya Nakuru wameelezea furaha yao ya kuunga mkono hatua ya mbunge wao Kimani Ngunjiri na spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika kuzika tofauti zao za kisiasa.
Wakaazi hao wamesema kuwa hatua ya Ngunjiri na Kihika kuungana itasaidia pakubwa katika kuleta maendeleo kwa kuwa wawili hao wataunganisha nguvu zao na maarifa yao katika kuwahudumia wakaazi wa Bahati.
Wakiongozwa na Bethuel Mbugua ambaye anatarajiwa kuania kiti cha uwakilishi wadi ya bahati mwaka 2017, wakaazi hao wamewataka Ngunjiri na Kihika kudumisha urafiki wao na kufanya kazi pamoja kuelekea mwaka 2017.
Wakiongea na mwandishi huyu,aidha wakaazi hao wamewataka viongozi wengine wa kaunti kuiga mfano wa wawili hao na kuungana kwa manufaa ya watu wa Nakuru.
“Sisi kama wakaazi wa Bahati tulifurahi kuwaona wakishikana mikono na kuapa kufanya kazi pamoja na tunawataka kudumisha ahadi yao ili waweze kutufanyia kazi,”alisema Mbugua.
Mwenyekiti wa maendeleo ya wanawke wadi ya kiamaina Tabitha Mwangi alimpongeza Kihika kwa kutoa mfano mwema wa maridhiano kama mama na kuwa taka viongozi kuheshimu kina mama wanaopigania nyadhifa za uongozi.
“Spika kihika ametoa mfano mwema kama kiongozi wetu nah ii inaonyesha kuwa kina mama wako tayari kufanya kazi na kila mtu bila kubaguana kwa misingi ya vyama ama hata kabila,” akasema.
Alimtaka spika Kihika kutumia wadhifa wake kuwaaunganisha viongozi wa kaunti ya Nakuru ili waweze kufanya kazi pamoja.