Share news tips with us here at Hivisasa

Wadau mbalimbali katika sekta ya utalii mjini Nakuru wanatarajia biashara yao iimarike zaidi hasua tunapoelekea kwenye shamrashamra za sikukuu ya krismasi.

Katika mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu jumanne, mkurugenzi mkuu katika hoteli ya Cathay iliyoko mjini Nakuru, Alfred Kitur alielezea matumaini yake ya kuimarika kwa sekta ya utalii huku akiitaja ziara ya mwaka huu ya kiongozi wa kanisa kotiliki duniani Papa Francis na ile ya rais wa marekani Barrack Obama kama zilizoimarisha imani ya wageni wa kimataifa wanaolenga kuzuru Kenya.

“Utalii hasua mjini Nakuru unazidi kuimarika ikilinganishwa na hapo awali. Huenda hatua hii inatokana na ziara ya rais wa marekani Barack Obama na kiongozi wa kanisa katoliki hapa nchini baba mtakatifu kwa kuwa imewapa motisha wageni kutoka ng’ambo kuzuru Kenya. Pia sisi tumeshuhudia ongezeko la watalii hapa Nakuru,” alisema Kitur.

Huku akikariri kuwa wanatarajia kuwa na shughuli nyingi mwezi huu wa desemba, Kitur pia ametaja juhudi za serikali za kuhamasisha maajenti wa usafiri na kuwahimiza wageni kuzuru Kenya kama miongoni mwa sababu ambazo huenda zikapelekea sekta ya utalii kuimarika hapa nchini.

“Serikali pia imetekeleza wajibu wake na pia imejibidiisha kuwahimiza wanaotoa tahadhari za kutozuru Kenya kuzifutilia mbali. Serikali pia imekuwa ikiwajuza wageni kwamb Kenya ni nchi salama tofauti na ilivyotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kwamba ni nchi inayolengwa na washambulizi ,’ aliongeza mkurugenzi huyo.

Aidha, Kitur ameongezea kuwa mikakati kambambe itawekwa na wadau mbalimbali kama njia ya kupiga jeki huduma inayotolewa kwa watakaozuru hoteli za kifahari hapa Kenya ikiwemo kupunguzwa kwa ada zinazotozwa kwa majumba na hoteli zinazotumika na wageni wanapozuru Kenya.

Haya yanaarifiwa huku mataifa ya ng’ambo yakianza kuruhusu wananchi wao kusafiri humu nchini kufuatia kuimarika kwa hali ya usalama hapa nchini.