Baada ya walimu kuitikia wito wa viongozi wa vyama vya kutetea haki za walimu nchini na kurejea shuleni, wengi wao kutoka kaunti ya Mombasa wametoa malalamiko kuwa bado hela za mwezi wa tisa hazijaingia kwenye akaunti zao kinyume na vile walivyoahidiwa na tume ya kuwaajiri walimu nchini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wameitaka serikali, kupitia tume hiyo, kuwawekea hela zao pamoja na marupurupu yao ili kuzitumia wanapoanza shughuli za masomo shuleni.

Baadhi ya walimu ambao waliongea na mwandishi huyu wa habari walisema kuwa bado hela zao hazijaonekana kwenye akaunti zao, licha ya ahakikisho kutoka kwenye tume ya TSC.

Mwalimu mmoja ambaye pia ni kiongozi wa jumuia moja ambayo huwapa walimu mikopo katika eneo la Likoni mjini Mombasa Ken Mwamburi alisema kufika siku ya Jumatatu mchana alikuwa amepokea malalamishi ya walimu wengi ambao walitaka kupigwa jeki ya mikopo kutoka kwa jumuia hiyo ambayo inaitwa Teachers Relief, na kusema kuwa wengi wao bado wana mahitaji ya kuwalipia wanao hela.

Mwamburi alitoa hisia zake kwenye serikali kuwatumia walimu hela zao ndio iwe motisha, ikizingatiwa kuwa bado wengine wana machungu kufuatia uasi ulioonyeshwa na tume ya TSC kuwalipa nyongeza yao.

James Mande, ambaye ni mwalimu wa moja ya shule ya za upili kutoka kaunti ya Mombasa, kwenye mahojiano katika mji wa Mombasa alisema kuwa aliamkia kazini lakini hakupata pesa, ikizingatiwa kuwa alihitaji hela ili kumfaa kwenye shughuli ya usafiri na mahitaji mengine kuenda na kurudi shuleni kutoka maskani anamoishi.

Lulu Hatimy, ambaye hufunza shule ya kimishenari ya Secret Heart, alithibitisha kuwa naye bado hajapokea hela kwenye akaunti yake. 

Akiongea nje ya benki moja mjini Mombasa alikokuwa amepiga foleni kuangalia hela, alitoa wito kwenye mamlaka husika kuangalia suala hilo na kuwatumia hela zao haraka na mapema ndio waanze shughuli zao vizuri.