Mwenyekiti wa kitaifa wa shirika la Kenya Women Grassroots Empowerment and Gender Equity Grace Kibuku ameonyesha kuhuzinishwa kwake na hatua ya kujiuzulu kwa Anne Waiguru kama Waziri wa Ugatuzi.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Jumatatu, Kibuku alisema kwamba Waiguru alitekeleza kazi yake vizuri kwa kuwahamasisha akina mama mashinani na pia kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakumba vijana.
“Kama mama, nimehuzunika sana kwa sababu Waiguru alizunguka kote nchini huku akiangalia nafasi ambazo anaweza kukuza, na pia akaweza kuwatambua akina mama ambao wamekuwa wakifanya kazi mashinani,” alisema Kibuku.
Kibuku alisema kuwa alikutana na Waiguru siku ya Ijumaa iliyopita katika hafla ya akina mama na kusema kwamba aliona afya yake ilikuwa imedhoofika.
Kutokana na hilo, aliema kwamba alitarajia Waiguru ajiondoe kwa muda kwenye nafasi ili uchunguzi ufanywe kuhusiana na madai ya ufisadi yanayokumba wizara ya ugatuzi.
Ingawa alisema kuwa ni vyema kuwa Waiguru alijiuzulu kutokana na sababu za kiafya, alisisitiza kwamba ni jambo la kuhuzunisha kwani Waiguru alikuwa mwenye bidii katika kutekeleza kazi yake.
“Nilitarajia ajiondoe kwa muda afisini na wala sio kujiuzulu. Hata hivyo, ni sharti awajibikie swala hilo kwani yeye ndiye alikuwa msimamizi wa Wizara ya Ugatuzi,” alisema Kibuku.
Matamshi yake yanajiri baada ya Waiguru, kujiuzulu siku ya Jumamosi kutokana na sababu za kiafya.
Kung’atuka kwake kulifuatia kashfa mbalimbali katika wizara ya ugatuzi kama vile ubadhirifu wa takriban shilingi milioni mia nane katika idara ya huduma kwa vijana NYS.