Shirika la kitaifa la idadi ya watu na maendeleo nchini NCPD limesifia idadi kubwa ya wanaume nchini ambao wameanza kukumbatia mbinu za kisasa za upangaji uzazi zinazolenga wanaume.
Kwa mujibu wa shirika hilo ni kwamba hali hiyo itachangia pakubwa uboreshaji huduma kwa jamii hasa familia za mapato ya chini.
Hatua hiyo inaoana na sera ya NCPD inayolenga kuona kwamba Wakenya wana idadi ndogo ya watoto ili wapokee huduma bora katika nyanja zote.
Shirika hilo lilisema ufanisi huo unatokana na uhamasisho ambao linazidi kuendeleza kote nchini kwa Wakenya wa matabaka yote.
Mkurugenzi wa huduma za kiufundi katika NCPD George Kichamu alisema wanaume wengi wamegundua umuhimu wa kupanga uzazi.
“Wanaume wamekuwa kiungu muhimu sana katika kampeini zetu za kuhamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi,wengi wao sasa ndio wanatembelea vituo vya afya kupokea huduma za kupanga uzazi” alisema Kichamu.
Akihutubia wanahabari kuhusu maswala ya upangaji uzazi mjini Eldoret aliwataka wanaume zaidi hasa kutoka katika maeneo kame kukumbatia mpango huo.
Kwa mujibu wa Kichamu ni kwamba idadi kubwa ya watu ambao wanaishi katika maeneo kame wangali nyuma katika mipango ya kupanga uzazi.
Kichamu alisema hali hiyo imechangia katika ongezeko la umaskini katika maeneo kame na maeneo ya mashambani kote nchini.
Shirika hilo linaendelea kushughulikia sera ambayo itafanikisha shughuli za mpango wa uzazi katika Nyanja zote kote nchini.