Zaidi ya watu 66,000 wanaugua ugonjwa wa Ukimwi katika Kaunti ya Nakuru, huku Visa vipya vingine 4,000 vya ugonjwa huo vikiwa vimebainika mwaka huu pekee.
Haya ni kulingana na mratibu mkuu katika shirika la NACC eneo la Central Rift, Hillary Chepsoror.
“Visa hivi huenda vimechangiwa na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake wanaofanya biashara ya ngono katika jimbo la Nakuru, haswa katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi ambayo inahusisha madereva wa magari aina ya masafa marefu, watalii na vile vile dhuluma za kijinsia miongoni mwa sababu zingine,” alisema Chepsoror.
Chepsoror, aliyeongea na wanahabari katika hafla ya kuadhimisha siku ya ukimwi duniani Jumanne alisema kuwa wengi wa waathiriwa wa ugonjwa huo ni vijana kati ya umri wa kiaka 9-35, huku akitaja kina dada kuwa walioathirika zaidi na ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa inafaa kuwa na haja ya kuwahamasisha vijana, hususan wa jinsia ya kike, kubaini hatari za ugonjwa huo na jinsi ya kukaa katika maisha ya ujana sawia na hata kubaini hali yao ili kuchukua hatua za tahadhari.
Wakati uo huo, amewaomba wazee ambao ametaja idadi yao kuwa haba kuzuru vituo vya kupimwa ugonjwa huo maarufu VCT ili kujua hali yao, na wala sio kuwaachia jukumu hilo kina mama.
Hata hivyo, imebainika kuwa asilimia 50 tu ya wakazi katika jimbo hilo ndio tu wanajua hali yao.
Ametaja kuwepo kwa mwongozo wa miaka mitano utakaolekeza zoezi litakaoloangazia ugonjwa huo wakizingatia jinsia ya kike kwa asilimia kubwa.