Wakazi kutoka eneo la Jogoo mjini Kisii wamemuua mnyama ambaye hajawahi kuonekana kwenye eneo hilo, na kushikwa na hofu kubwa kuwa huenda mnyama huyo akawa wa mganga au wa kutumiwa na masuala ya kichawi.
Mnyama huyo ambaye ana sura sawasawa na mlandano wa kimo kama kile cha cha mamba aliuliwa mchana wa siku ya Jumatatu, baada ya watoto kumpata kwenye ploti moja ya kuishi katika eneo hilo, na kupiga kamsa ambapo wakazi walijumuika na kumpiga mawe na kufa papo hapo.
Kulingana na Nemuel Maina, ambaye ni mkazi kwenye ploti hiyo, mnyama huyo alipatikana na mmoja wa watoto wa ploti hiyo, ambaye alikuwa ameenda kuoga bafuni ambapo alimwona akitambaa kwenye kijishamba kimoja kilichoko jirani na mmoja wa mwenye boma iliyo jirani ambapo alipiga kelele na kuwaita wakazi kwenye ploti hiyo.
“Mtoto wa jirani alikuwa ametoka shuleni na akaelekea bafuni kuenda kuoga, ambapo alishtuka kumwona mnyama kimo kikubwa sampuli hiyo ambaye hajawahi kuonekana katika sehemu hii ya Kisii, ilibidi watu wakakusanyika na kupiga na kumuua,” alisema Maina.
Naye Faith Mokaya, ambaye pia ni mkazi, alisema kuwa hajawahi kumwona mnyama kama huyo, ila mnyama aina ya mjusi pamoja na mamba ambao wanakuwa na sura sawia na mnyama huyo na kuongeza kuwa mamba hajawahi kuwa mbali na maeneo ya maji.
Mama huyo aliwalaumu baadhi ya wakazi katika sehemu hiyo ambao hujihusisha na masuala ya uganga kuwa huenda ndio washukiwa ambao walimleta mnyama huyo hapo, na akatoka kutafuta chakula na kujipata mahali pasio salama kwake.
Hata hivyo, mmoja wa wajuzi wa masuala ya wanyama James Ondari ambaye amepata kuishi sehemu mbali mbali nchini alisema kuwa mnyama huyo huenda alitolewa Mombasa kwa sababu wanyama sampuli hiyo hupatikana sana Mombasa na hufahamika kwa lugha la Kizungu kama 'Monitor Lizard'.
Mnyama huyo ameuliwa siku mbili tu baada ya joka moja mkubwa kuuliwa siku ya Jumamosi katika eneo la Nyambera kwa kupigwa risasi, kisa ambacho wakazi hawajashuhudia hata siku moja.