Kamanda wa trafiki katika eneo la Bonde la Ufa Bi Mary Omari ametoa wito kwa madereva wa magari ya usafiri wa umaa kupunguza safari za usiku msimu huu wa krismasi.
Omari alisema kuwa hatua hiyo itakuwa njia moja ya kupunguza idadi ya ajali za barabarani zinazotokea nyakati za usiku.
Omari alisema kuwa idadi kubwa ya ajali za barabarani hutokea usiku, jambo ambalo amesema linaweza kuepukwa kwa kupunguza idadi ya safari zinazofanywa usiku.
Akiongea afisini mwake siku ya Jumanne alipokutana na wawakilishi wa wamiliki magari mjini Nakuru, Omari alisema kuwa madereva wengi hupuuza sheria za trafiki na hata alama na ishara za barabarani wanaposafiri usiku.
“Katika barabara kuu ya Nairobi-Eldoret ajali nyingi hutokea usiku na hii inasababishwa na utovu wa nidhamu miongoni mwa madereva wetu. Tunataka tujaribu kupunguza safari za usiku haswa kwa watu wanotoka Nairobi kuelekea magharibi mwa nchi na wale wanaosafiri kwenda Nairobi ili tuweze kupunguza idadi ya ajali,” alisema Omari.
Bi Omari alisema kuwa idara ya trafiki imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret haswa mwezi huu wa Disemba.
“Mambo mengi hufanyika sana Disemba lakini kama idara, tuko tayari kuhakikisha kuwa usalama barabarani unadumishwa na Wakenya wanasafiri salama,” alisema Omari.
Afisa huyo aliwataka madereva kuzingatia sheria za trafiki na kukumbuka kuwa wanaowabeba katika magari yao ni binadamu.