Mke wa Gavana wa Kaunti ya Nyamira Bi Naomi Nyagarama amewahimiza wanawake wajawazito walio na mazoea yakujifungulia nyumbani kuasi tabia hiyo nakuanza kujifungulia kwenye zahanati na hospitali za umma.
Akihutubia wakazi katika uwanja wa Nyamaiya, Bi Nyagarama alisema kuwa idadi kubwa ya kina mama ambao huaga dunia ni wale wanaojifungulia nyumbani.
"Idadi kubwa ya kina mama ambao hufariki kutokana na matatizo yakujifungua ni wale wanaojifungulia nyumbani, kwa kuwa hawapati huduma muhimu jambo la dharura linapotokea," alisema Bi Nyagarama.
Aidha, aliwaomba wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja huo wa Nyamaiya kumkaribisha Bi Margaret Kenyatta siku ya Jumatano atakapozuru kaunti hiyo kupeana kliniki ya kina mama kujifungua.
"Bi Kenyatta atazuru kaunti hii siku ya Jumatano na ninawaomba wakazi mjitokeze kwa wingi kumkaribisha kwenye uwanja huu kwa kuwa anakuja na habari nzuri zakutuletea kliniki tamba itakayo wasaidia pakubwa kina mama wajawazito," alisema Bi Nyagarama.