Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ameahidi kuzindua mradi wa kuwasajili wanafunzi kiteknolojia na kuripoti moja kwa moja kwa mzazi ili kusitisha visa vya ukosefu wa nidhammu miongoni wa wanafunzi.
Kulingana na Nassir, wazazi wengi wamekuwa wakilalama kuhusu watoto wao kurejea nyumbani kuchelewa baada ya masomo, hali ambayo imewatia hofu wazazi wengi kukosa kufahamu wanachokifanya wanao baada ya masomo.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita mjini Mombasa siku ya Jumanne, Nassir amesema kwamba mradi huo utasaidia kuwepo na mawasiliano ya moja kwa moja baina ya walimu na wazazi katika kutambua mienendo ya wanafunzi ili kuwaepusha na kujihusisha na uhalifu, mihadarati na mimba za mapema.
“Mradi huo tutakaouzindua utawawezesha wazazi kuwasiliana moja kwa moja na walimu katika kufahamu mienendo ya watoto wao. Nadhani mfumo huo wa teknolojia utasadia pakubwa kuzuia wanafunzi kujihusisha na visa vya utovu wa nidhamu,” alisema Nassir.
Aidha, amehoji kuwa kwa ushirikiano baina ya walimu, wazazi na viongozi, basi swala la elimu katika eneo bunge hilo litaimarika kwa kiwango kikubwa kwani eneo hilo linatambulika kwa kuchangia misukusuko ya ukosefu wa usalama humu nchini.
“Tukishirikiana vyema, basi viwango vya elimu katika eneo bunge la Mvita vitaimarika pakubwa na juhudi za wanafunzi zitaonekana. Kwa hivyo ni lazima kwa watoto wetu kupata msingi bora wa elimu ili kuwasaidia kujiepusha na visa vya utovu wa nidhamu,” aliongeza Nassir.
Mapendekezo ya Mbunge huyo yamejiri baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hukwepa masomo shuleni na kujihusisha na maswala ya misimamo mikali na utumizi wa mihadarati hali ambayo imedidimiza viwango ya elimu.