Kamishena wa kaunti ya Nyamira Josphene Onung’a amesema wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa katika kaunti hiyo, haswa katika shule mbalimbali.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatatau mchana katika mji wa Nyamira, kamishena huyo alisema wanahitaji kuwahusisha wakuu wote wa shule mbalimbali zilizoko katika kaunti hiyo kwa usalama ili shambulizi lolote lisije likatekelezwa katika kaunti hiyo.
“Hatutaki kushuhudia shambulizi lolote kwa shule za kaunti yetu ya Nyamira kama lile shambulizi lilillotekelezwa katika chuo kikuu cha Garissa, ndio maana tunahitaji kuwahusisha wakuu wa shule kwa usalama na kuwafundisha jinsi ya kujua washambulizi au kikundi cha ugaidi kabla hawajatekeleza shambulizi lolote,” alihoji Onung’a.
“Kama njia mojawapo ya kuporesha usalama kwa shule zetu, sharti tuwape wakuu wa shule mafunzo ya kiusalama na kujua kila kitu ambacho kitawafanya kujua watu wabaya,” aliongezea Onung’a.
Wakati huo huo, alisema kila mwanafunzi katika kaunti hiyo lazima ajulikane hutoka wapi, kama njia moja ya kuimarisha usalama kwa kaunti hiyo.
Aidha, kamishena huyo alisema kila mtu, haswa wale wakuu wa shule wakipokezwa mafunzo ya kujua jinsi washambulizi huonekana, kisa chochote cha mashambulizi hakiwezi kushuhudiwa katika kaunti hiyo.
Kwa upaande mwingine, wakaazi wa kaunti hiyo walionekana kufurahishwa na mikakati hiyo ya kamishena, na kusema usalama utaimarishwa ipasavyo .
“Hayo matamshi ya kamishena wetu ameyasema kutekelezwa kwa wakuu wa shule zetu kwa kuwapa mafunzo ya kiusalama tunayaunga mkono,” alisema Elijah Nyanduri, mkaazi.