Wakazi wa Wadi ya Sensi wamemuomba mwakilishi wao Ochong’a Nyagaka, kuwawekea mradi wa maji katika wadi hiyo.
Kulingana na wakazi hao, mwakilishi huyo aliwaahidi hapo mbeleni kuwa atawawekea miradi ya maji katika kila sehemu ya wadi, kama njia moja ya kuwarahisishia kazi ya kutembea masafa marefu wakitafuta maji.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika eneo la Sombogo, wakazi hao wakiongozwa na Andrew Nyansongo, walisema mwakilishi wao aliwaahidi kuwawekea miradi ya maji katika baadhi ya sehemu kwa kuwachimbia visima vya maji na kufikia sasa hakuna lolote wameliona likifanywa.
“Tunamuomba mwakilishi wetu kutuwekea mradi wa maji katika wadi yetu. Yeye ndiye alitoa ahadi na sisi sharti tuifuatilie ahadi hiyo ili aweze kuitimiza,” alisema Nyansongo.
“Ni mwaka mmoja tangu mwakilishi wetu aahidi kutuwekea mradi wa maji katika eneo la Nyakeiri. Tunashangaa ni nini kimemchelewesha kutimiza ahadi hiyo. Tunaomba atimize ahadi hiyo kwa sababu tunateseka kwa kutembea masafa marefu tukitafuta maji,” alisema Grace Nyambati, mkazi.