Idara ya trafiki katika Kaunti ya Nakuru imesema kuwa itafanya msako wa pikipiki za bodaboda kutokana na ajali nyingi zinazofanya.
Idara hiyo aidha imesema kuwa ukosefu wa kuvalia kofia ya usalama na kutozingatia sheria zilizowekwa barabarani umechangia pakubwa kuongezeka kwa ajali zinazosababishwa na pikipiki hizo.
Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Hassan Barua amedhibitisha kuwa pikipiki hizo zinahitilafiana na kanuni za barabara, na kuwa wengi wa waendeshaji hawazingatii kanuni zilizowekwa.
Kamanda huyo alikuwa akizungumza baada ya kufanya kampeini ya usalama wa barabara katika eneo la Kinungi kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru.
“Tutafanya msako huo wakati wowote, na wale watakaopatikana watashtakiwa na kupoteza leseni zao za kuhudumu,” alisema Barua.
Naye msimamizi wa mamlaka ya kusimamia babarabara kuu nchini (KeNHA) Ezekiel Fukwo aliongeza kuwa wameweka mikakati maalum ili kuhakikisha kuwa ajali zimepungua haswa wakati huu wa sherehe nyingi, na baadaye.