Bunge la kitaifa limetakiwa kusisitiza kutumika kwa sheria ya jinsia ili kumpa mwanamke nguvu katika uongozi.
Akizungumza siku ya Alhamisi, kwenye hoteli moja jijini Mombasa wakati wa kongomano la viongozi wa wanawake, Waziri wa masuala ya nje Amina Mohammed ,alisema wanawake wanapaswa kupewa nafasi za uongozi katika mashirika mbalimbali.
Bi Mohammmed alisisitiza kuwa sheria ya jinsia inafaa kutekelezwa ili kumpa mwanamke nguvu katika uongozi.
Aliongeza kwa kusema kuwa wanawake bado wanakosa nyadhifa muhimu katika mashirika na serikali kwa jumla.
Waziri huyo alitoa mfano wa wizara yake kwa kusema kuwa katika wizara hiyo, asilimia 47 ya maafisa ni wanawake na asilimia 58 ikiwa ni ya wanaume.
Alisema kuwa lengo lake kuu ni kuweka usawa.
Aidha, ametaka elimu ya mtoto wa kike kupewa kipao mbele humu nchini, kwa kusema kuwa elimu kwa wasichana itatengeneza nafasi nzuri kwa mwanamke na kumpa uwezo wa kujiamini katika uwajibikaji na maendeleo ya taifa.