Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti imeombwa kuanzisha taasisi ya kukuza vipaji katika Kaunti ya Kisii ili kuinua na kukuza talanta za vijana na kuwawezesha kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha kupitia vipaji hivyo.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya vijana wana vipaji lakini wanakosa nafasi ya kukuza talanta hizo.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika uwanja wa Chuo kikuu cha Kisii ambapo kongamano la wafanyibiashara litaandaliwa kwa siku tatu kuanzia siku ya Alhamisi, kundi la vijana, likiongozwa na Samuel Ogeto na Teresa Robi liliomba serikali ya Kisii kujaribu kila iwezalo kuwasaidia vijana walio na vipaji kujiendeleza kwa kuanzisha taasisi ya kukuza vipaji katika kaunti hiyo.

“Ukweli wa mambo ni kuwa kuna ukosefu wa taasisi za aina hiyo hapa Kisii, na tunaomba Gavana James Ongwae ikiwa anajali maslahi ya vijana aanzishe taasisi ya kukuza vipaji ili tuweze kujiendeleza kupitia talanta zetu,” alisema Ogeto.

“Serikali ya Kisii imekuwa ikitoa ahadi za kujenga taasisi hiyo na tayari miaka ile ambayo tuliahidiwa imekamilika. Tunaomba serikali kutimiza ahadi hiyo haraka,” alisema Robi.