Viongozi wa kaunti ya Tana River wamepinga vikali madai ya kuwa jamii ya Wapokomo katika kaunti hiyo wamekuwa wakisajiliwa kuwa wafuasi wa kundi lililoharamishwa la Mombasa Republican Council MRC.
Mwenyekiti wa Chama cha Mzalenzo Abdallah Bwanamaka amesema kuwa madai hayo ni ya uvumi ili kuwachochea wakazi wa eneo hilo kuzua rabsha na kuvurugu mipango ya uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Bwanawaka amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotumia vyombo vya habari kwa kuwapa habari za kiuchochezi ili kusababisha taharuki katika kaunti hiyo, ilhali jamii hiyo haina uhusiano wowote na kundi hilo la MRC.
Aidha, amekiri kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wanaochochea madai hayo pamoja na wanahabari wanahongwa kutoa habari za kichochezi na kuchangia taharuki katika jamii hiyo ili maafisa wa polisi kuwavamia na kusababisha uhasama usiotarajiwa na jamii hiyo.
"Jamii ya Wapokomo haina uhasama na mtu yeyote, lakini kuna baadhi ya wanasiasa wanaochochea serikali kuwa jamii ya wapokomo inasajiliwa na kundi la MRC kuwa wafuasi wao ili kuzua vurugu katika kaunti ya Tana River, hilo sio kweli na tutasimama kupigiania watu wetu kwa sababu sio wahalifu," alisema Bwanamaka.
Amesema kuwa jamii hiyo iko mstari wa mbele kueneza amani na kuwashauri wenzao kujisajili kuwa wapiga kura na kuchagua viongozi waadilifu.
Amewaonya viongozi wanaowachochea wakazi kukoma mara moja kuwaharibia sifa jamii ya wapokomo kwani ni watu wakupenda amani.
Picha: Mwenyekiti wa Chama cha Mzalenzo Abdallah Bwanamaka akiwaonya viongozi wanachochea jamii za wapokomo katika kaunti ya Tana River na kuzua vurugu kuwa watawachukulia hatua za kisheria. Bwanamaka/twitter