Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shirika moja la wanaharakati wa kisiasa wameisifia bodi ya uajiri ya bunge la kaunti ya Nyamira kwa kuzingatia uwazi katika shughuli zake za kuwaajiri wa wafanyikazi.

Kulingana na mwenyekiti wa Nyamira Transparency Group Stella Kerubo, shirika hilo halijawahi kupokea malalamishi kutoka kwa wananchi kuhusiana na ufisadi pamoja na mapendeleo katika kuwaajiri wa wafanyikazi.

" Ningependa kuipongeza bodi ya uajiri wa wafanyikazi katika bunge la kaunti ya Nyamira chini ya uongozi wa spika Joash Nyamoko kwa kuwa hatujapokea malalamishi kutoka kwa wananchi kuhusiana na mapendeleo na ufisadi wakati wa kuwaajiri wafanyikazi na hiyo ni ishara tosha kuwa wananchi wanaimani na bodi hiyo," alisema Kerubo. 

Hata hivyo, Kerubo alisema kuwa bodi ya uajiri wa wafanyikazi kwenye kaunti ya Nyamira ambayo imekuwa ikishutumiwa kwa madai ya ufisadi inafaa kuiga mfano wa bodi ya uajiri ya bunge la kaunti hiyo ili kurejesha imani ya wananchi. 

"Tunafahamu kuwa kuna wakati ambapo bodi ya uajiri wa wafanyikazi katika kaunti ya Nyamira ilikuwa karibu kubanduliwa na serikali ya kaunti hiyo hadi pale mahakama ilipoamru makamishna wa bodi hiyo kurejea kazini na huenda sababu ikawa mapendeleo kwenye uajiri na kwa kweli wananchi wengi wamekuwa wakiwasilisha malalamishi ya ufisadi na mapendeleo dhidi ya bodi hiyo."

"Ushauri wangu kwa bodi hiyo nikuiga mtindo wa bodi ya uajiri bungeni kwa minajili yakurejesha imani ya wananchi," aliongezea Kerubo.