Gavana wa Kaunti ya Kisumu Jack Ranguma, amepewa changamoto kuzuru mitaa ya mabanda jijini Kisumu, ili kufahamu matatizo wakazi wa mitaa hiyo wanayokumbana nayo.
Mwenyekiti wa Kisumu City Informal Settlements Network (KISNET) Eliezar Osanya, alisema kuwa Ranguma anafaa kuzuru mitaa hiyo kama hatua ya kumwezesha kutatua changamoto za wakazi hao.
Kwenye kikao na wanahabari mtaani Manyatta siku ya Jumatano, Osanya alisema kuwa wakazi wa mitaa ya mabanda wanakabiliwa na changamoto si haba, ambazo sharti serikali ya Kaunti ya Kisumu itatue.
“Barabara mbovu, nyumba duni, ukosefu wa mabomba ya kupitisha maji taka na ukosefu wa maji safi ya matumizi ni miongoni mwa matatizo yanayotukumba sisi kama wakazi wa mitaa ya mabanada,” alisema Osanya.
Aidha, Osanya alikashifu mpango wa serikali ya Kaunti ya Kisumu kutumia shilingi milioni 38 kuwajengea nyumba wakazi wenye mapato duni katika wadi mbalimbali za jimbo la Kisumu.
Alisema kuwa hawakufahamishwa kuhusu mpango huo, na ni sharti wafahamishwe na kushirikishwa kikamilifu kwenye juhudi hizo.
Wakazi wa mitaa ya mabanda jijini Kisumu wanatarajiwa kukutana siku ya Alhamisi mtaani Nyalenda, kwa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki za binadamu ulimwenguni.
Mwenyekiti huyo wa KISNET alisema kuwa kauli mbiu yao wakati wa maadhimisho hayo, ni Makao Bora, Haki Yetu.
Miongoni mwa mitaa hiyo ni Obunga, Nyalenda, Manyatta, Otonglo, Bandani na Manyatta Arabs.