Mwakilishi wadi ya Flamingo kaunti ya Nakuru Moses Gichangi ameshtumu vikali kundi la vijana waliowahangaisha wenzao kwa mashambulizi ya mapanga na ametoa wito kwa vijana katika mtaa wa Flamingo kuwa watulivu na kutumia fursa za hazina mbalimbali kijiimarisha kibiashara badala ya kuzua vurugu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumzia suala la kundi la vijana hao kuzua fujo mtaani Flamingo usiku wa kuamkia leo, MCA Gichangi amesema kuwa wengi wa vijana waliohusika katika uvamizi huo hawana ajira na ni kutokana na hilo ambapo wanaamua kujiingiza katika masuala ya uhalifu.

"Ningependa kuwaomba vijana tafadhali tusiwe watu wa kuzua rabsha na vurugu na badala yake tutumie fedha kutoka hazina mbalimbali za serikali kuhakikisha tunajiimarisha," alisema Gichangi.

Wakati uo huo, Mwakilishi wadi huyo ametoa wito kwa idara ya polisi kuimarisha doria katika mtaaa huo wa Flamingo ili kukabiliana na wale wanaojaribu kuzua rabsha.

Kwa mujibu wake, wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu, kuna umuhimu wa kueneza amani na kuepuka malumbano ambayo huenda yakayumbisha kaunti ya Nakuru na taifa kwa jumla.