Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa Mombasa wanailaumu idara ya usalama wa kupokonywa walinzi kwa gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho.

Wakazi hao wakiongozwa na Athuman Ali, mkazi wa Magongo, walisema siku ya Alhamisi kuwa hatua hiyo inavunja imani kwa wananchi wa Mombasa ikizingatiwa gavana wao anapaswa kupewa usalama kwa mujibu wa katiba.

Athuman ameitaka idara hiyo kumhakikishia usalama wa kutosha gavana Joho ili kuepuka kushambuliwa.

Hatua hii inajiri baada idara ya polisi nchini kumpokonya gavana Joho walinzi wake saba, huku kaimu mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Patrick Njoroge akija kuwachukua maafisa hao bila ya kumueleza sababu ila kusema ni amri kutoka kwa wakubwa wake.

Saba hao ni pamoja na maafisa wawili waliokuwa wakilinda nyumbani kwake, wawili waliokuwa afisini na watatu aliokuwa akizunguka nao.

Kitendo hicho kimesadifiana na kauli ya Marwa hapo awali akiwa Kwale akisema huenda baadhi ya walinzi wa wanasiasa hapa pwani wakachukuliwa hatua kwa kutumiwa vibaya na wanasiasa kuwashambulia na kuwajeruhi wananchi.

Marwa alidai walinzi hao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi na hata kuwajeruhi hasa wale wanaowapinga viongozi hao.

Aidha alieleza kwamba walinzi hao walitumika vibaya kuwanyanyasa raia wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi.

Joho amepuuzilia mbali madai hayo na kusema amepokonywa walinzi kwa misingi tu ya kisiasa.

Picha: Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho. Amepokonywa walinzi wake na idara ya polisi, huku wananchi wakionyesha kutoridhiswa kwao. Maktaba