Halmashauri ya Bandari nchini KPA, inatarajiwa kukagua zabuni zilizotumwa na baadhi ya makampuni kutoka nchi 15 za Afrika na Ulaya ili kupewa nafasi ya kandarasi ya ujenzi wa eneo la kuegesha meli la Kipevu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano katika bandari hiyo, zoezi hilo la kukagua zabuni hizo limeanza rasmi na kampuni itakayoidhinishwa itaanza ujenzi huo mwezi Julai mwaka huu.

Taarifa hiyo imesema kuwa eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuegesha meli zaidi ya nne.

Aidha, eneo hilo litakuwa na upana wa kuweka makasha hata zaidi ya laki mbili kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara katika nchi za bara la Afrika na Ulaya.

Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa KPA pia itajenga barabara ya Dongo Kundu pamoja na kuunganisha upya mabomba ya mafuta kutoka eneo la Bandari ya Mombasa hadi Kipevu, kama njia moja wapo ya kuimarisha shughuli za biashara na ukuzaji uchumi wa nchi.

"Tumeanza zoezi la kukagua maombi ya zabuni yaliyotumwa na baadhi ya makampuni kutoka nchi 15 za Afrika na Ulaya, kabla ya kupewa nasafi ya kuanza kandarasi hiyo ya ujenzi mwezi Julai,” alisema Hajj Masemo, kwenye taarifa hiyo iliyotumwa siku ya Jumanne.

Kampuni zilizotuma maomba ni kutoka taifa la Uingereza, Afrika Kusini, Uchina, Japan, India, Dubai, Marekani, Uholanzi pamoja na mataifa mengine.