Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kukemea tamaduni ya kuwakeketa wasichana.

Akizungumza afisini mwake siku ya Jumanne, alipompokea mwenyekiti wa bodi yakukabili ukeketaji wa wasichana nchini Jebii Kilimo, Gavana Nyagarama alisema kuwa yeyote atakaye patikana akiendesha tamaduni hiyo potovu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

"Nimeunga rasmi vita dhidi ya ukeketaji wa wasichana na yeyote, awe mzazi au mhudumu wa afya, atakaye patikana akiendesha tamaduni hiyo iliyopitwa na wakati, atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Nyagarama.

Nyagarama alipongeza mashirika ya kijamii pamoja na makanisa kwa kuendeleza kampeni hiyo, huku akionya wazazi dhidi yakuwaoza wanao kabla yao kuhitimu umri unao hitajika.

"Ningependa kuyashukuru mashirika ya kijamii na pia makanisa kwa kuunga mkono kampeni yakupinga ukeketaji. Makanisa ya kiadventista na katholiki yamedhihirisha mfano mwema katika vita hivyo na sasa ni himizo langu kwa wazazi, kuhakikisha kuwa wanakumbatia ushauri wa mashirika hayo, ili kuwawezesha wasichana kupata elimu kwa minajili yakujistawisha maishani. Wacha hili liwe onyo kwa wazazi wanao ruhusu mabinti wao kuolewa kabla yakuhitimu umri ufaao," alisema Nyagarama.