Sharti kila mtu na jamii kwa jumla kuchukua nafasi ya kukabiliana na ugaidi pamoja na itikadi kali miongoni mwa vijana nchini Kenya, ili kuleta uwiano miongoni mwa dini zote nchini.
Haya ni kulingana na shirika la Brave ambalo linakabiliana na itikadi kali miongoni mwa vijana nchini.
Shirika hilo limewataka wazazi kuungana na kupiga jeki juhudi za shirika hilo katika kuwakuza watoto wao katika mienendo mizuri ya kufuata dini.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika mkahawa wa watalii wa Nyali Beach, katika kongomano la kuwahamasisha wazazi kuhusu itikadi kali, mwenyekiti wa kamati kuu ya shirika hilo, Sheikh Ibrahim Lethome, alisema kuwa sharti wazazi wawajibikie malezi ya wanao ili kuhakikisha kuwa vijana wanakua katika maadili mema.
Shirika hilo la Brave ambalo limeanzisha harakati za kuwahamasisha vijana pamoja na wazazi dhidi ya ugaidi na itikadi kali miongoni mwa jamii, limewataka viongozi pamoja na wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kuona kuwa wanakua katika njia sawa na kuwapa msaada wanapouhitaji.
Mkutano huo ambao ulianza siku ya Jumatano utaendelea kwa siku tatu na unatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa.
Miongoni mwa masuala ambayo yanalenga kujadiliwa ni pamoja na kutafuta mbinu mwafaka za kuwafikia vijana na kuwahimiza jinsi ya kujiepusha na makundi haramu ya kigaidi na itikadi kali miongoni mwa mengine.