Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha kutetea haki za wapangaji mjini Eldoret kimeonya kwamba huenda kukatokea mkurupuko wa maradhi mjini humo.

Chama hicho kilisema kuna hatari ya kutokea kwa mkurupuko wa maradhi kutokana na uchafu katika mitaa mbalimbali mjini humo haswa msimu huu wa mvua.

Kulingana na chama hicho, wamiliki wa nyumba katika mji huo hawazingatii usafi wa nyumba zao.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimetaka wamiliki wa nyumba hizo kuchukua hatua za dharura kuimarisha usafi katika nyumba zao.

Akizungumza mjini Eldoret, Katibu wa chama hicho, Bw Benard Nandwa, alisema chama chake hakitasita kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa ploti ambazo hazina vyoo na mazingira safi.

“Hali imekuwa mbaya zaidi msimu huu wa mvua. Miongoni mwa mitaa inayokumbwa na hali duni ya usafi ni Langas, Huruma, Kamukunji na Munyaka,” alisema Nandwa.

Baadhi ya wapangaji katika mita hizo wametishia kususia kulipa kodi ya nyumba ikiwa wamiliki wa nyumba hizo hawataimarisha usafi katika ploti zao.

Tayari idara ya afya ya umma katika mji wa Eldoret imeanzisha msako dhidi ya wamiliki wa ploti ambazo hazina vyoo na raslimali zingine za kudumisha usafi mjini humo.