Vijana katika eneo bunge la Kisauni wamehimizwa kujiunga katika makundi na kusajili makundi hayo ili waweze kupewa pesa za kuanzisha miradi za kujikimu kimaisha.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba alisema kuwa vijana wengi katika eneo la Pwani hungoja kuajiriwa katika Bandari ya Mombasa na katika ofisi mbalimbali za serikali.
Alisema kuwa hali hiyo imepelekea vijana wengi kukaa bila ajira kwa kukosa kutafuta mbinu zingine za kupata riziki.
“Leo hii nawaahidi kuwa ikiwa mtajiunga katika makundi na kusajili makundi hayo, basi mtapata pesa za kuanza miradi kama vile uvuvi wa samaki ambao unafanya vyema sehemu nyinginezo,” alisema Bedzimba.
Mbunge huyo wa Kisauni pia alisema kuwa ukosefu wa ajira umechangia pakubwa vijana kujihisisha na uhalifu na pia utumizi wa mihadarati.