Katibu wa chama cha Wiper Democratic Party tawi la Nyamira Victor Ogeto amejitokeza kuutaka muungano wa CORD kufanya uchaguzi wa kitaifa ili kuwapa wakenya nafasi ya kumchagua kiongozi atakaye peperusha bendera ya muungano huo kwenye uchaguzi mkuu ujao. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ogeto alisema kuwa iwapo muungano wa CORD utazingatia ushauri wa kuwapa wakenya nafasi ya kumteua mmoja wa vinara wa CORD kuwania urais hiyo itakuwa njia mojawapo ya kusaidia chama hicho kufanya kampeni zake kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

"Ningependa kuwapa changamoto vinara wa muungano wa CORD kuwapa nafasi wakenya kumteua mmoja wao kwenye kura ya siri kwa hali hiyo itatusaidia pakubwa kuushinda muungano wa Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao na nina hakika kwamba mbinu hii itatusaidia kuwafikia watu wengi na kuwauzia sera za muungano wetu," alisema Ogeto. 

Ogeto aidha alisema kwamba iwapo pendekezo lake litatekelezwa, kiongozi atakayeshinda kwa kupata kura nyingi kwenye maeneo ya kaunti atapata nafasi ya kupeperusha bendera.

"Pendekezo hili ni zuri na linatumika kule Marekani na tayari nimeandikia barua bodi kuu ya muungano wa CORD ili kuona iwapo watalitekeleza kwa maana tutapata wagombezi kulingana na idadi ya wajumbe watakaowapigia kura na hivyo hivyo yule atakaye pata wajumbe wengi ndiye atakayepewa tiketi ya muungano wa CORD," aliongezea Ogeto. 

Akizungumzia suala la baadhi ya wajumbe kuchagua viongozi kwa kutowahusisha wengine, Ogeto alisema kuwa hatua hiyo hukandamiza haki za wajumbe wengine kutoka sehemu mbalimbali nchini.

"Sio vizuri kwa wajumbe wengine kupendelewa zaidi ya wengine ili kuwachagua viongozi kwa niaba ya wananchi na sharti maamuzi yetu yaamuliwe na wafuasi wa vyama tanzu vya CORD," alisisitiza Ogeto.