Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa amewataka viongozi kutoka Pwani walioasi chama cha ODM kujiuzulu nyadhifa zao mara moja.
Jumwa ametaja hatua hiyo ya kugura ODM kama uasi mkubwa ikizingatiwa wakaazi waliwachagua kupitia chama hicho.
Alisema kuwa ikiwa viongozi hao wameamua kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta basi wanapaswa kukiunga chama cha Jubilee kikamilifu na kustaafu kwani afisi wanazoongoza kwa sasa walizipata kupitia chama cha ODM.
Bi Jumwa alisema ataungana na viongozi kutoka Pwani kuwahamasisha wenyeji kuhusiana na uasi huo wa viongozi kuanzia kaunti ya Kilifi, Mombasa na Kwale, ili kuhakikisha kuwa wakaazi wanawatambua vyema viongozi wenye hulka za kubadlisha msimamo wao.
Akizunguma katika eneo bunge la Malindi, Jumwa alisema kilichosalia ni kuandaa mikutano na madiwani ili kuhakikisha kuwa wanaupigia upato mrengo wa Cord eneo nzima la Pwani, haswa Kaunti ya Kwale, ambapo wakaazi walishangazwa na hatua ya gavana kuhamia mrengo wa Jubilee.
Alisema ni muhimu kurejesha amani kwa wenyeji kuwa Cord itajitahidi kushinda kwenye uchaguzi ujao.
Hata hivyo, ametoa wito kwa viongozi wenzake wa chama cha ODM kuwa waaminifu kwenye mrengo wa Cord ili kuleta maendeleo katika eneo la Pwani.