Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Meneja msimamizi wa kampuni ya usambazaji umeme nchini KPLC, tawi la Nyamira, amejitokeza kuelezea sababu yakupotea kwa nguvu za umeme mara kwa mara katika kaunti hiyo.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari afisini mwake siku ya Jumatano, meneja huyo, Dancan Machuka, alisema hali ya kupotea kwa nguvu za umeme katika maeneo mengi Nyamira husababishwa na mvua nyingi inayoendelea kunyesha.

Alisema kuwa hali hiyo inasababisha baadhi ya nyaya za umeme kukatika kwa kuangukiwa na miti.

"Tumekuwa tukishuhudia changamoto za kupotea kwa nguvu za umeme huku Nyamira kutokana na mvua nyingi inayoendelea kunyesha. Mvua hiyo huangusha miti na kisha kukata nyaya za umeme," alisema Machuka.

Machuka vilevile aliwasihi wakazi wa kaunti hiyo kuasi tabia yakupanda miti karibu na nyaya za umeme akisema kuwa miti hiyo huenda ikasababisha uharibifu mkubwa wa nyaya hizo na hata pia kuwasababishia wenyeji maafa.

"Umeme ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa na kwasababu hiyo, nawahimiza wananchi kuasi tabia ya kupanda miti karibu na nyaya za umeme kwa kuwa miti hiyo kuweza kuanguka nakukata nyaya hiyo," alisema Machuka.

Akizungumzia swala la matepeli kuendelea kuwahadaa wananchi kuwa wao ni mawakala wa kampuni hiyo ya usambazaji umeme, Machuki aliwasihi wananchi kuwa macho nakuripoti visa vyovyote vya aina hiyo kwa polisi, pindi wanaposhuku kuwa mawakala hao sio halali.

"Tumekuwa tukipokea ripoti kuwa kuna watu ambao wamekuwa wakiwatapeli wananchi kwakudai kuwa wao ni mawakala wa Kenya Power. Ningependa kuwahimiza wananchi kuchukua tahadhari kuhusiana na watu wa aina hiyo nakuchukua hatua yakupiga ripoti mara moja kwa maafisa wa polisi,” alisema Machuka.