Wakazi wa mtaa duni wa Manyani ulioko mjini Nakuru sasa wanaiomba serikali ya kaunti kumnasa muuzaji mkuu wa pombe haramu mtaani humo kama njia moja ya kupunguza unywaji na uuzaji wa pombe hiyo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi hao ambao walisema wamechoshwa na pombe hiyo waliiomba serikali kuwatumia kumnasa muuzaji huyo, ambaye anajulikana kwa majazi kama 'Anyole'.

Walisema 'Anyole' amekua akiuza pombe hiyo kwa mda mrefu, na hakuna hatua yoyote imewahi chukuliwa dhidi yake. 

Waliongeza kuwa muuzaji mkuu huyo anawauzia vijana pombe bila kuzingatia sheria zilizomo, huku akijigamba kama mfanyibiashara mashuhuri mtaani humo. 

Wakazi hao ambao waliongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi walisema wake kwa wanaume hushinda maasaa ishirini na manne wakibugia pombe hiyo bila kukamatwa na polisi ambao tayari washafaamishwa kumhusu muuzaji huyo. 

Walilalamikia pia usalama wao wakisema muuzaji huyo uletewa pombe masaa ya saa kumi na moja asubuhi na watu wasiojulikana wanaotumia magari ya kibinafsi kusafirisha pombe hiyo. 

Eunice Wanja, mkazi wa mtaa huo alisema wanawe wawili wa kiume wamepotelea nyumbani kwa muuzaji huyo, ambapo wao hushinda wakinywa pombe na kuja tu nyumbani kulala. 

Wanja aliongeza kuwa watu wasiopungua hamsini hushinda kwenye boma hilo lililoko karibu na makaburi ya Nakuru South Cemetary, mita chache kutoka kituo cha kibiashara cha Manyani.

"Vijana wangu wamepotelea uko kwa 'Anyole', ambapo wao hushinda wakinywa pombe. Ningeomba serikali imkamate kwani ameharibu vijana wengi sana hapa mtaani," alisema Wanja.

Wakazi hao wametishia kuvamia boma hilo iwapo serikali ya kaunti haitamchukulia muuzaji huyo wa pombe haramu hatua hivi karibuni.