Wananchi walio na leseni za kumiliki bunduki wameonywa dhidi ya kuzitumia bunduki hizo visivyo, la sivyo wakabiliwe vikali kisheria.
Kamanda wa polisi wa kawaida katika jimbo la Kisumu Nelson Njiri ameonya kuwa yeyote aliye na kibali cha kumiliki bunduki ataadhibiwa endapo atakwenda kinyume cha sheria ya matumizi ya bundiki.
“Ikiwa una leseni ya kumiliki bunduki na unaitumia visivyo, utakabiliwa na hatua kali ikiwemo kupokonywa bundi hiyo,” alionya Njiri.
Akizungumza jijini Kisumu siku ya Jumanne, Njiri alisema kuwa idara ya polisi imepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu baadhi ya watu wanaomiliki bunduki kuwatishia maisha wananchi wapenda amani.
Kauli ya Njiri ilijiri huku maafisa wa kitengo cha CID wakiendelea kumsaka meneja wa hazina ya Kustawisha eneo Bunge la Nyando (CDF), aliyeingia mafichoni baada ya kudaiwa kumpiga risasi na kumuua mlinzi mmoja katika eneo la Burudani mjini Ahero.
Meneja huyo anadaiwa kumpiga risasi na kumuua mlinzi huyo usiku wa siku kuu ya Krisimasi.