Eneo la Ukunda, Pwani limetajwa kuongoza kwa visa vya biashara ya ngono miongoni mwa watoto, huku zaidi ya visa 400 vikiripotiwa.
Katika ripoti ya kuatua nyoyo, ni zaidi ya watoto 400 katika eneo hili wanaohusishwa na biashara hii na walezi wao na hata watu wao wa karibu.
Takwimu za ripoti ya uchunguzi ya shirika la Terre Des Hommes, linaloendeleza hamasa za kuwanasua watoto dhidi ya biashara hii na kuwafadhili, zinaonyesha kwamba idadi hii huenda ikaongezeka.
Kulingana na Kahaso Pendo, mshirikishi wa mipango katika shirika la SCOPE amesema kwamba utalii na umaskini ndio chanzo cha watoto kushirikishwa katika ngono biashara.
Aidha, amewalaumu waekezaji katika sekta ya utalii kwa kuwatumia watoto kama kitega uchumi katika biashara zao.
Watoto waendeshaji bodaboda vile vile hawajasazwa katika kuchangia biashara hii.
Watoto hawa wenye kati ya umri wa miaka 9 hadi 12, hutumiwa pia na watalii na baadhi ya wakaazi katika biashara ya kutengeza filamu za ngono.
Maeneo ya mangwe sasa yametajwa kama yaliokithiri na biashara hii huku serikali ikitakiwa kukaza kamba katika kudhibiti maeneo ya burudani.
Sera za kukabili visa hivi katika ngazi za kaunti, pia zilitajwa kuwa hafifu hali inayodaiwa kusababisha biashara hii kuendelea na kukosa kudhibitiwa kisheria.
Wakati huo huo, wazazi waliombwa kuwajibikia malezi ya watoto wao ili kukomesha visa hivi.