Seneta wa kaunti ya Nyamira Okongo Mongare amejitokeza kushtumu mpango wa serikali ya Jubilee kutaka kupokeza shule za msingi za umma vipakatalishi.
Akihutubu wakati wa kupeana tarakilishi kwa shule ya upili ya Don Bosco siku ya Jumanne, Mongare alisema yafaa serikali itumie pesa inazonuia kununua vipakatalishi ili kuinua hadhi kwenye maabara ya tarakilishi kwenye shule za umma.
"Sio eti kwamba napinga hali ya kutaka kufanya masomo kwenye shule zetu za msingi ila baadhi ya miradi hasa ya kuwapokeza wanafunzi wa darasa la kwanza, vipakatalishi ni mchezo na huu mpango wao wa kuwapa wanafunzi ni ishara kuwa serikali haijaweka mikakati ya kuimarisha elimu," alisema Mongare.
Mongare aidha alisema kuwa uimarishaji wa maabara ya tarakilishi kwenye shule za upili za umma utaipunguzia mzigo serikali, huku akihoji kuwa wanafunzi wanaotoka katika shule za msingi watapata nafasi ya kusomea masuala ya tarakilishi pindi tu watakapo jiunga na shule za upili.
"Itaiwia rahisi serikali ya Jubilee kuimarisha maabara ya tarakilishi katika shule za upili kwa maana shule hizo ni chache ikizingatiwa na idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza wanaonuiwa kupokezwa vipakatalishi hivyo na uzuri ni kwamba wanafunzi hao watapata nafasi ya kusomea masuala ya tarakilishi pindi watakaopojiunga na kidato cha kwanza," aliongeza.
Akizungumzia swala la kuajiri watalaam zaidi kwenye shule za upili za umma, Mongare alisema kuwa yafaa serikali iwaajiri walimu wa masuala ya tarakilishi ili kutoshelesha mahitaji ya wanafunzi.
"Vilevile tunaitaka tume ya walimu nchini TSC kuwaajiri walimu wa taaluma ya tarakilishi ili kusaidia wanafunzi kupata mafunzo ya tarakilishi na hiyo itakuwa njia mojawapo yakubuni nafasi za ajira," alihoji Mongare.