Kesi ya uchochezi inayomkabili Seneta wa Tana River Ali Bule imehairishwa kwa muda.
Seneta huyo aliwasilisha ombi katika mahakama kuu, la kutaka Hakimu Diana Mochache kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa kusema kuwa hakimu huyo alimpa masharti makali ya dhamana.
Hii ni baada ya mahakama kuu kuagiza kusimamishwa kwa kesi hiyo kwa muda, hadi pale uamuzi utakapotolewa kuhusiana na ombi la wakili wa seneta huyo, la kutaka Hakimu Mochache kujiondoa kwenye kesi hiyo na kupunguzwa kwa masharti aliyopewa.
Hakimu Mochache alikuwa amewagiza Seneta Bule kutozungumzia kuhusu kesi hiyo katika vyombo vya habari na kwenye mikutano ama makongamano hadi pale kesi hiyo itakapotamatika.
Aidha, Mochache alimpiga marufuku Bule kutozuru eneo la Kanagoni, Kaunti ya Kilifi, ambako jamii ya Wagiriama inaishi hadi kesi yake itakapotamatika.
Bule anadaiwa kutoa matamshi ya uchochezi na chuki yanayodaiwa kuvuruga amani baina ya jamii mnamo Julai 15, 2015, katika ukumbi wa Hurura, kaunti ndogo ya Garsen.
Mahakama kuu inatarajiwa kutoa uamuzi wake Disemba 15, 2015.