Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi kutoka maeneo mbali mbali hasa maeneo ya Likoni na Mtongwe wamepongeza hatua ya wizara ya uchukuzi kumsimamisha kazi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la feri Hassan Musa, ambaye alisitishwa majukumu yake siku ya Jumatano.

Wakazi hao sasa wamesema kuwa ni muda mwafaka kwa serikali kuingilia kati na kutafiti kilichosababisha masaibu pamoja na matatizo ya mara kwa mara yaliyolikumba shirika hilo, hasa kukwama kwa feri ambazo zilisababisha watumizi wengi kubaki na maswali.

Wakiongea siku ya Alhamisi na mwandishi huyu katika kivuko cha Likoni baada ya kupokea habari za kusimamishwa kazi kwa Hassan, Nulla Aboud ambaye aliongea kwa niaba ya watumzi wa kivuko hicho alisema kuwa hiyo hatua imekuja ikiwa imechelewa kwani mkurugenzi huyo alihitajika kufutwa kazi kitambo.

Aidha alisema kuwa wengi wamefurahi kuondolewa kwa afisaa huyo mkuu ambaye alimtaja kuwa asiyejali masilahi ya wakazi wa maeneo ya Likoni na Mtongwe pamoja na wateja wa kila siku wa kivuko hicho na kumshukuru waziri wa uchukuzi James Macharia.

Walitoa wito kwa meneja mpya wa shirika hilo kutofuata mtindo wa mtangulizi wake na kuanza kupigana na maovu yote yaliyoachwa humo na kuhakikisha kuwa shirika hilo linarejelea hadhi yake ya zamani ili kuwapa imani wateja ambao wengi wao huleta kipato kwenye serikali kama vile watalii ambao utembelea eneo maarufu la Diani huko South Coast.