Mwanasiasa katika eneo la Masaba, Bw Ratemo Nyara, ameonya vijana didi ya siasa duni, zinazorudisha maendeleo ya jamii ya Kisii nyuma.
Akizungumza siku ya Jumatano katika Wadi ya Kiamokama, Ratemo alisema kuwa vijana wamekuwa wakitumika na wanasiasa na watu wa nia mbaya kuharibu mali na maendeleo ya jamii hiyo.
Ratemo alisema kati ya miradi ambayo vijana wameonekana wakiharibu ni barabara ambazo wanadai ziko katika hali ambayo haipitiki.
“Hivi majuzi vijana walichimba mtaro katika barabara ya Kiamoka-Ibacho, na kutatiza uchukuzi katika eneo hili kwa siku kadhaa,” alisema Ratemo.
Mwanasiasa huyo amewarai vijana kutokubali kutumiwa na viongozi walio na siasa ya kubomoa wala sio ya kujenga.
Aliahidi kutangamana na vijana katika miradi ya maendeleo katika eneo hilo.
Kundi la vijana, likiongozwa na Elijah Kieri, liliwaonya viongozi dhidi ya kutowajibika kikazi na kuwataka kuanzisha kutekeleza miradi ya maendeleop katika eneo hilo.