Wahudumu wa afya katika Kaunti ya Nakuru wamesema huenda wakagoma baada ya hatua ya kupandishwa vyeo kucheleweshwa, na pia kutokana na hatua ya kukosa kulipwa marupurupu.
Akizungumza kwa mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa chama cha kutetea madaktari cha Kenya Medical Practitioners and Dentists Union (KMPDU) kwenye kanda ya Kusini mwa Bonde la Ufa, Dkt Austin Oywer, alisema kwamba wahudumu wa afya 96 na washauri wanaofanya kazi katika vituo mbalimbali vya kiafya kwenye kanda hiyo ya bonde la ufa wako katika mgomo baridi.
Oywer alisema kuwa mgomo huo baridi ulianza siku ya Jumatano na huenda wakafanya mgomo kuanzia siku ya Ijumaa iwapo matakwa yao hayataafikiwa.
Kulingana na Oywer, wakati wa majadiliano miezi minne iliyopita, walikubaliana na maafisa wa kaunti ya Nakuru wakiongozwa na Naibu Gavana Joseph Ruto kuwapandisha vyeo madaktari ambao wamehitimu lakini hilo halijaafikiwa kwa sasa.
Alisema kwamba kufikia sasa, ni madkatari watatu tu ambao wamepandishwa vyeo chini ya mradi wa kuboresha uchumi, huku akisisitiza kwamba ni sharti tarehe ya kuwapandisha vyeo isongezwe nyuma ili iambatane na tarehe ambayo wangefaa kupandishwa vyeo.
Aidha, alisema ni lazima wapewe marupurupu yao kulingana na wakati huo ambao utasongezwa nyuma.
Oywer alisema kwamba iwapo Kaunti ya Nakuru haitatekeleza matakwa yao kufikia siku ya Ijumaa, watashiriki katika mgomo.
Kulingana naye, wamewapoteza zaidi ya madaktari 10 kutokana na motisha wao kuwa chini.