Afisa wa afya ya umma kwenye Kaunti ya Nakuru Dkt Samuel King'ori amedhibitisha kuwa ni sawa kwa nyama ya punda kuliwa na binadamu.
Kwenya mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Jumatano, King'ori alisema ilani iliyotolewa mwaka wa 2010 chini ya sheria zinazoongoza ubora wa nyama inataja punda kama mnyama anayeweza kuliwa sawa na wanyama kama vile mbuzi na kondoo.
“Nataka kutoa dhibitisho kuwa nyama ya punda ni nyama iliyo nzuri. Hii ni kulingana na ilani 110 ya tarehe 16 Julai mwaka wa 2010 ambayo iliwekwa kwenye gazeti la serikali kuwa nyama ya punda inaweza kuliwa. Ni mojawapo ya wanyama waliowekwa kama wanaofaa kuliwa na binadamu,” alisema King’ori.
Hata hivyo, afisa huyo wa afya ya umma alisema tatizo kuu ni kuwa wanaouza nyama hii hukosa kuwafahamisha wananchi kuwa nyama wanayonunua ni ya punda.
Aidha, alisema kuwa baadhi ya wanaouza nyama hiyo pia hukosa kuchukua leseni kutoka kwa ofisi ya afya ya umma ya kuwaruhusu kuuza nyama hiyo.
“Changamoto ni kutokana na njia ambazo watu hutumia katika kuuza nyama ya punda. Wengine huiba wanyama hao, jambo ambalo ni hatia. Jambo lingine ni kuwa wanyama hao huchinjwa katika eneo lisilofaa. Isitoshe, wauzaji huwa hawafichui kuwa nyama wanayouza ni ya punda, jambo ambalo pia ni kinyume cha sheria,” alisema King’ori.
Wakati huo huo, alitaja ufunguzi wa kichinjio cha punda mjini Naivasha kama jambo la busara akiashiria kuwa iwapo kichinjio hicho kitapata leseni kutoka kwa afisi ya afya ya umma kwenye Kaunti ya Nakuru, basi watakubaliwa kuuza nyama hiyo.
Ni matamshi ambayo huenda yakawa afueni kwa wakaazi wa eneo la Chemongoch katika eneo la Mogotio Kaunti ya Baringo, ambao mwaka jana walihimiza serikali kupitia kwa wizara ya kilimo na uvuvi kutoa leseni kwa kiwanda cha kuchinja punda kilicho katika eneo hilo.
Wakaazi hao walisema tangu kiwanda hicho kilipojengwa, zaidi ya miaka matatu iliyopita, wamefaidika pakubwa kwa njia mbalimbali kama vile kupitia ajira na kwa kupata maji kupitia kwa bwawa ambalo lilichimbwa hivi maajuzi.