Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kushirikiana kikamilifu na serikali ya kitaifa ili kuwafaidi wavuvi pamoja na wafanyabiashara wa samaki, na wanaisihi serikali kukumbatia samaki badala ya kuendelea kuagizia samaki kutoka mataifa ya kigeni.

Kwenye mahojiano siku ya Jumanne na Ahmed Kassim, kiongozi wa kundi moja la kusambaza samaki kwa wenye mabanda ya samaki jijini Mombasa, bei ya samaki inaendelea kudidimia kwa sababu ya kuletwa kwa samaki wengine kutoka maeneo kama vile Tanzania.

Kiongozi huyo amedai kuwa imefika wakati serikali kuu kutambua sekta ya uvuvi pamoja na washika dau wa idara hiyo kwa jumla kwa kuwapa kipaumbele, na kuwahusisha kwenye maamuzi muhimu yanayowahusu kwenye suala zima la uvuvi na usambaji wa samaki kwenye masoko ya humu nchini.

Kassim pia ametoa lawama kubwa kwa idara za kushughulikia sekta hiyo kama vile ile ya uvuvi pamoja na wizara husika kwa kukosa kudhibiti na kuweka utaratibu mwafaka ambao utawanufaisha wahusika ambao mara nyingi huhangaika kuingia majini kuvua na kuhakikisha kuwa samaki anamfikia mteja.

Aliongeza kudai kuwa wale wanaofaidi kutoka sekta hiyo ni mawakala ambao wamekuwa wakinunua samaki kwa bei ya chini na kusafirisha kuenda miji mingine kama Nairobi, na kuuza katika mikawa mikubwa kwa bei mara tano zaidi walivyoinunua.