Wakimbizi wa ndani kwa ndani mjini Subukia wamesema kwamba uchaguzi ujao unawatia hofu na wasiwasi mkubwa, kama hawatakuwa wamepata fidia kutoka kwa serikali.
Matatizo yanayokabili wakimbizi hao hisani wa katika kaunti ndogo ya Subukia Nakuru, aidha yamefanya baadhi ya watoto wao kuwa wa mtaa.
Mwenyekiti wao George Njoroge, amesema tangu waende Subukia wakati walifurushwa makwao 2007/2008 baada ya vita kuzuka kufuatia uchaguzi ulioleta utata nchini, serikali imewatelekeza na sasa wanafungiwa nyumba.
“Hatukwenda katika hema kwa sababu tulisaidiwa na marafiki tukapata mahali pa kukaa, lakini baadaye wakaanza kutulipisha hizo nyumba. Miaka tisa sasa inatimia na hatujaona usaidizi wa serikali. Uchaguzi mwingine umefika na tuko ugenini. Tumeshindwa kulisha watoto, kuwapeleka shule, na sasa wengine wamekuwa chokoraa,” alisema bwana Njoroge.
Bi Jane Njogu alisema: “Tunafukuzwa kwenye nyumba hizo kwa kushindwa kulipa. Maisha yetu ni ya shida kwa sababu hata tukipata kibarua cha 200, mwenye shamba anakupimia mara mbili ya kipimo cha kawaida. Akina mama sasa wanatoroka na kuacha mabwana zao na watoto wakirandaranda mitaani.”
Walikuwa wakizungumza na wanahabari mjini Nakuru Jumatano.