Kizaaza kilishuhudiwa kwenye la Bunge la Kaunti ya Kisumu siku ya Alhamisi, baada ya wawakilishi wa wadi waliokuwa bungeni kupata habari kwamba meneja wa jiji la Kisumu Dorris Ombara, alikuwa ameachishwa kazi katika hali ya kutatanisha.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Kamati ya Watoto, Jinsia na Utamaduni katika Bunge la Kaunti ya Kisumu, ambaye pia ni mwakilishi wa Wadi ya Nyakach Kusini Mashariki Petronilla Omondi, wawakilishi hao walisema kuwa hawatakubali Ombara kuachishwa kazi bila sababu kutokana na utenda kazi wake bora.
“Hatutakubali Dorris Ombara kuachishwa kazi bila sababu kutokana na utendakazi wake bora. Wananchi wengi katika kaunti hii wanakubali kazi ya Ombara na kama ni lazima aondoke, sharti tuelezwe nini kimefanyika,” alisema Bi Omondi.
Barua ya kumuachisha kazi Ombara, inadaiwa kutoka kwenye afisi ya katibu wa serikali ya Kaunti ya Kisumu.
Kelvin Oraro, ambaye ni mwakilishi wa Wadi ya Kolwa Magharibi, alidai kuwa Ombara anapigwa vita na baadhi ya watu kwenye serikali ya Kaunti ya Kisumu.
Alimtaka katibu wa serikali ya Kaunti ya Kisumu, kujitokeza wazi wazi kueleza sababu ya Ombara kuachishwa kazi kwenye mazingira ya kutatanisha.
“Ugomvi ulianza pale afisa mmoja kwenye serikali ya Kaunti ya Kisumu alipodinda kutoa pesa za kumuwezesha Dorris Ombara kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Katibu wa kaunti anafaa kujitokeza haraka kutueleza kile kinachofanyika,” aliongeza Oraro.