Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kisii Chris Obure amewaomba wakazi wa kaunti hiyo kushika vitambulisho vya kitaifa na kadi za kupiga kura kwa wingi kabla ya uchaguzi mkuu ujao ili kupata fursa ya kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo.

Ombi hilo lilitolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wakazi ambao wamehitimu umri wa miaka 18 bado hawana vitambulisho vya kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari alhamisi mjini Kisii, Obure alisema kila mkenya anastahili kuchagua kiongozi ampendaye na atakayeleta maendeleo, huku akiwaomba wakazi kujitokeza kwa wingi na kushika kadi hizo.

Wakati huo huo, Obure aliwaomba wakazi ambao tayari wanavitambulisho vya kitaifa na bado hawajajisajili kama wapiga kura kufanya hivyo kwa wakati mwafaka.

Obure alisema kila mkazi anaposhika kitambulisho cha kitaifa ahakikishe pia amejisajili kama mpiga kura ili  kushiriki uchaguzi mkuu wa 2017.

“Nawaomba wakazi ambao wamefikisha umri wa miaka 18 na zaidi katika kaunti yetu ya Kisii kujiandikisha kupata vitambulisho vya kitaifa na kadi za kupiga kura ili tupate uogonzi bora,” alisema seneta huyo.

“Uongozi wa maendeleo sharti uletwe na wapiga kura ili kunufaika ifikapo mwaka wa 2017 wakati kura zitaandaliwa kote nchini,” aliongeza Obure

Pia Obure alisema chama cha ODM kimejitayarisha vilivyo kutembea kila eneo bunge la kaunti ya Kisii kwa wiki mbili sijazo ili kuelimisha wakazi umuhimu wa kupiga kura .