Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeombwa kuajiri wasimamizi wa vijiji ambao watasimamia vijana watakaofanya miradi ya maendeleo vijijini, haswa upanuzi wa barabara.

Hii ni baada ya serikali ya kaunti hiyo ya Nyamira kutenga shillingi millioni 30 kufanya maendeleo kama vile upanuzi wa barabara na miradi ya maji.

Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama alisema kuwa serikali ya kaunti itawaajiri vijana 20 katika kila ili kufanikisha miradi hiyo.

Akizungumza siku ya Jumatano katika wadi ya Nyansiongo, mwakilishi wa wadi hiyo Jackson Mogusu alisema itakuwa vizuri kwa serikali kuajiri wasimamizi katika vijiji, watakaosimamia vijana ambao watafanikisha miradi ya maendeleo katika vijiji hivyo.

“Ikiwa serikali inahitaji kutoa usaidizi kwa watu wetu ili kupata sabuni ya kila siku, sharti iwajiri wasimaimizi wa vijiji ambao watasimamia miradi ya maendeleo. Wakazi watasaidika sana kupitia hatua hiyo,” alisema Mogusu.

Mapema wiki hii, Gavana Nyagarama aliahidi kuleta maendeleo zaidi katika sehemu zote za kaunti, ili kunufaisha wakazi wa kaunti.