Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi kutoka kijiji cha Eburru, eneo la Gilgil, walifanya maandamano siku ya Alhamisi kulalamikia barabara mbovu katika eneo hilo.

Wakaazi hao walidai kuwa wamesahaulika na serikali kwa muda mrefu tukio ambalo limewaacha wakitaabika mara kwa mara.

Kulingana nao, barabara za eneo hilo zimekuwa hazipitiki na kulaumu serikali za kaunti ya Nakuru na hazina ya CDF ya Gilgil kwa kukosa kushughulikia masaibu yao.

Wakiongozwa na mmoja wa kiongozi wa kijiji hicho, Lydia Nyota, wakaazi hao walisema kuwa licha ya kupata usaidizi kutoka kwa kampuni zinazopakana na kijiji hicho, hakuna msaada waliopata kutoka kwa serikali ya kaunti.

“Wengi wetu tunaadhirika na mvua inayoendelea kunyesha kwa kuwa inaharibu barabara hata zaidi. Tunataka hatua za dharura zichukuliwe na serikali ya kaunti pamoja na hazina ya CDF ya eneo bunge la Gilgil,” alisema Nyota.

Peter Mbugua, mkazi, alisema kuwa eneo hilo hukuza megawati tano ya kawi ya mvuke na inafaa kushughulikiwa kama maeneo mengine nchini.