Kamishna wa huduma za forodha katika mamlaka ya utozaji ushuru nchini Julius Musyioki amesema kwamba kwanzia Januari mwaka ujao makasha yote yanoingia katika bandari ya Mombasa yatakaguliwa na kupitisha kwa muda mfupi.
Katika mahojiano ya kipekee na mwanahabri huyu mjini Mombasa siku ya Alhamsi, Musyioki amesema kwamba shughuli hiyo itakuwa ikitekelezwa kwa muda wa masaa 12 badala ya siku tatu kama ilivyo kwa sasa.
Amesema kwamba shughuli hiyo inatarajiwa kupunguza misongamano ya makasha katika bandari hiyo, huku akisema kwamba kucheleweshwa kwa ukaguzi na kupitishwa kwa makasha kunazidisha gharama ya juu kutoka kwa wafanyibiashara wa kuleta na kusafirisha bidhaa kupitia bandari hiyo.
“Tumelenga wafanyibiashara wa kuleta bidhaa na kusafirisha nje ya nchi, kwa asilimia 70 tutapunguza misongamano hiyo kwani shughuli yote itakuwa inafanywa kwa muda wa masaa 12 badala ya siku tatu kwani wafanyi biashara watalazimika kujaza fomu zao za ukaguzi kupitia kwa mtandao,” alisema Musyioki.
Kwa upande wake Meneja wa KRA, tayari notisi imetolewa kupitia kwa vyombo vya habari kwa wafanyibiashara wote wa kuleta na kusafirisha bidhaa nje ya nchi ili wafahamu na mapema kuhusu mpango huo.
Hata hivyo, amehoji kuwa wafanyibiashara wa kibinafsi na wale wa makampuni mpango huo utawasaidia kupunguza gharama za utozaji ushuru pamoja na kucheleweshwa kwa bidhaa zote katika bandari hiyo ya Mombasa.