Mwanamke mwenye umri wa miaka 22, aliyetaka kumtia mwanawe wa wiki moja kisimani aliangua kilio alipokuwa akitoa ushahidi mbele ya mahakama ya Mombasa.
Shantel Samir Matano, alitiwa mbaroni katika eneo la Tudor-Moroto mnamo Julai 23, mwaka huu, baada ya kudaiwa kupatikana akitaka kumtia mtoto huyo kisimani.
Shantel aliwaacha wengi na mshangao alipo angua kilio na kusema madai yanayomkabili si ya ukweli bali ni njama ya kumpokonya mwanawe.
“Sio kweli, hii ni njama ya kunipokonya mwanangu,” alisema Shantel.
Shantel alisema alimuacha mwanawe chumbani akiwa amelala na kuenda kuuza nguo ili kupata riziki ya kumlea mwanawe.
“Nilimuacha mwanangu akiwa amelala, nikaenda kufanya biashara yangu ya kuuza nguo. Nliporudi nikaowaona majirani wakiwa wamemchukua mwanangu na kunisingizia eti nilitaka kumtia kisimani,” alisema Shantel.
Aliongeza kuwa iwapo alikuwa na nia ya kumuua mtoto huyo, basi angefanya hivyo hata kabla ya kumzaa, ikizingatiwa mchumba wake alikana kulea ujauzito huo.
Alisisitiza kuwa anampenda mwanawe sana na wala hawezi kufikiria kumuua.
“Kamwe sitoweza kufikiria kumuua mwanangu kwani nampenda na nitamlea vizuri,” alisema Shantel.
Hakimu mkuu Teresia Matheka atatoa uamuzi wake tarehe Oktoba 6, 2016.