Share news tips with us here at Hivisasa

Mwalimu mkuu wa Shule ya upili ya Maseno Paul Otula, ameonyesha furaha kufuatia watahiniwa waliofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne (KCSE) shuleni humo mwaka jana, kuandikisha matokeo mazuri.

Otula alisema kuwa walivuna matokeo mazuri kutokana na bidii ya wanafunzi na walimu.

“Bidii ndio imetufikisha hapo tulipofika. Ila nataka kuomba wadau husika kuimarisha miundo msingi katika shule hii, kwa sababau baadhi ya miundu msingi ni duni,” alisema mwalimu huyo aliyekuwa amejawa furaha.

Mtahiniwa mmoja shuleni humo aliorodheshwa katika nafasi ya tatu kote nchini.

Felix Nyabuto alipata A ya alama 84, na kuorodeshwa wa tatu kote nchini na wa kwanza katika eneo la Nyanza.

Watahiniwa 140 walipata A, watahiniwa 122 wakapata alama ya A-, 19 alama ya B+, watatu alama ya B na mmoja alama ya B-.

Punde tu baada ya kupokea matokeo hayo, wanafunzi wa shule ya upili ya Maseno walielekea kanisani kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Matokeo hayo ya mtihani wa KCSE wa mwaka jana, yalitangazwa mapema siku ya Alhamisi na waziri wa elimu Dkt Fred Matiang’i.

Watahiniwa zaidi ya laki tano walifanya mtihani huo kote nchini mwaka jana.