Wakazi wa Nakuru sasa wanataka tume ya kukabiliana na ufisadi iharakishe uchunguzi wake kuhusiana na mkopo wa Eurobond.
Hii ni kutokana na ripoti za kukanganya kutoka kwa upande wa serikali na ule wa upinzani kuhusiana na jinsi fedha hizo zilivyotumika huku serikali ikidai kwamba hakuna fedha abazo zilifujwa huku upande wa upinzani ukipinga usemi huo wa serikali.
Ni usemi ambao unajiri huku EACC ikiwa tayari imewahoji baadhi ya maafisa walio kwenye wizara ya fedha kuhusiana na sakata hiyo ya mkopo wa Eurobond.
"Eacc wanatakiwa kumaliza uchunguzi haraka na kuwajuza wakenya kuhusiana na matokeo ya uchunguzi wao. Watakaopatikana na hatia wanafaa kuchukuliwa hatua kali kwani Kenya kumekuwa na sakata nyingi za ufujaji wa fedha ilhali hakuna Yule ambaye tumeona akitakiwa kulipa fedha hizo," alidokeza Joseph Waweru mkazi wa Nakuru.
Aidha, wakaazi wengine waliozungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru Alhamisi tarehe 17 Desemba wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kujitokeza waziwazi kueleza ukweli wa mambo wakisisitiza kwamba matamshi yake ya siku ya Jamuhuri kwamba endapo fedha hizo zilifujwa watakaopatikana watachukuliwa hatua waliwaacha na maswali chungu nzima.
"Ni ombi langu kwa rais Uhuru Kenyatta kama mkenya kuingilia kati na kutatua tatizo hili. Rais Uhuru Kenyatta ni ishara ya umoja wa kitaifa na hivyo basi anafaa kuongelea sakata hiyo kwa mapana ili wakenya waijue na pia walio nje ya Kenya wafahamu ukweli wa sakata hiyo," alikariri Robert Omondi, mkazi mwingine wa Nakuru.
Wakaazi wengine wa Nakuru waliozungumza na mwandishi huyu hata hivyo wamesisitiza kwamba hawafahamu bayana kuhusiana na sakata hiyo ya mkopo wa Eurobond.
"Ukiwauliza wakenya kuhusiana na Eurobond, hakuna anayefahamu haswaa kuhusiana na swala hilo kwani wamekuwa tu wakiwasikia viongozi wakitupiana maneno kuhusiana na mkopo huo," alisema John Kimiti, mkazi mwingine.
Katika maadhimisho ya siku ya Jauhuru Desemba tarehe 12, Rais Uhuru Kenyatta pia alisema iwapo madai ya Kiongozi wa upinzani kwamba fedha hizo zimefujwa yatapatikana kuwa ni ya uongo, basi kiongozi huo anafaa kuchukuliwa hatua za kisheria.